IBIHUHA.COM

Friday, July 2, 2010

Nipeni mitano mingine 'nifunike' zaidi- Rais Kikwete

MGOMBEA pekee wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Rais Jakaya Kikwete ameomba apewe nafasi ya kuongoza nchi kwa miaka mitano mingine ili afanye kazi aliyoianza vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa awamu ya kwanza.

Rais Kikwete ameyasema hayo jana kwenye Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi mjini hapa, wakati aliporejesha fomu yake ya kuomba uteuzi wa chama hicho kwa ajili ya kupeperusha bendera yao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Rais Kikwete aliyewasili saa 5:06 katika Viwanja vya Makao Makuu ya CCM, alipokelewa na viongozi mbalimbali wa chama wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Pius Msekwa huku akishangiliwa na wanachama wa CCM waliokuwa wamevalia mavazi ya rangi ya kijani na njano.

Alilakiwa na vikundi mbalimbali vya burudani huku wakiimba nyimbo za kumsifu na kumpongeza Rais Kikwete wakiongozwa na bendi ya TOT chini ya Kapteni John Komba.

Alipofika sehemu aliyopangiwa, Rais Kikwete alipokewa na Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliyezihakiki fomu za mgombea huyo na kuridhia kuwa zilijazwa kwa umakini na kisha kuzipokea rasmi fomu hizo na kuthibitisha ndiye mgombea pekee.

Akizungumza muda mfupi baada ya kukabidhi fomu zake, Rais Kikwete ambaye atapigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, Julai 10, alisema kipindi cha miaka mitano kimekwisha na alifanya kazi nzuri na kuomba apewe nafasi ya miaka mitano mingine ili afanye kazi nzuri zaidi.

“Kazi ya Urais haina elimu ni kujiamini au kuaminiwa. Nimefanya kazi miaka mitano, miaka miwili ilikuwa ya kujifunza na miaka mitatu nikafanya kazi nzuri mnayoiona, mkinipa sasa miaka mingine mitano haitakuwa ya kujifunza ila kufanya kazi nzuri zaidi…naahidi mkinichagua nitafanya kazi vizuri kuliko awamu ya kwanza,” alisema Rais Kikwete.

Alisema wenye sifa ya kugombea nafasi hiyo ya urais ndani ya CCM ni wengi na hawana mapungufu, lakini hakuna aliyejitokeza kwa kile alichoeleza kumheshimu na kuwa na imani na uongozi wake.

Alisema ni imani yake kwamba Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa itampitisha katika Mkutano Mkuu kama mgombea wao na kwamba matumaini Watanzania watamchagua tena.

“Mafiga matatu yalitusaidia uchaguzi uliopita, nasema yatatusaidia tena. Nawaomba wanachama wenzangu mniunge mkono na kunichagua ili nifanye kazi hii tena,” alisema Rais Kikwete ambaye akichukua fomu Juni 21, mwaka huu, aliahidi kuwa akichaguliwa tena, atawatumikia Watanzania kwa Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi ili kuwaletea maisha bora.

Rais Kikwete alimshukuru kipekee mtoto wake, Ridhiwani kwa kushirikiana na wenzake kutembeza fomu nchi nzima kumtafutia wadhamini na kuonesha kushangazwa na watu waliokuwa wakihoji kwa nini amemtumia mwanawe kufanya kazi hiyo.

“Wako waliouliza kwa nini Ridhiwani, na mimi nikauliza kwa nini asiwe Ridhiwani. Nataka kusema kugombea urais ni jambo nililoamua mwenyewe sio chama, kwa hiyo lazima nifanye juhudi zangu binafsi kutafuta wadhamini kwa hiyo kumtumia mwanangu ambaye ni mtu wa karibu…halikuwa tatizo,” alifafanua Rais Kikwete akizungumzia timu hiyo ya vijana 32 iliyoongozwa na mwanawe.

Alisema wako watu waliodai amewadharau viongozi wa wilaya, kata na vijiji, hoja aliyoipinga na kueleza kuwa jukumu la viongozi hao ni kuandaa watu watakaomdhamini, lakini jukumu la kuzunguka kutembeza fomu kuomba udhamini ni la mgombea, hivyo anamshukuru Ridhiwani, marafiki zake na vijana kwa kubeba mzigo huo na kufanya kazi nzuri.

Alisema hatasahau wema na mchango wa kila mtu wakiwemo marafiki zake walioongoza vijana kutafuta wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, makatibu wa mikoa, wilaya, kata na matawi kwa kuandaa wanachama waliomdhamini na kwamba pale walipopunguza, wataongezewa na Mungu.

Naye Makamba alisema alishatabiri siku ya kwanza kuwa dalili zilikuwa zinaonesha Kikwete ndio mgombea pekee.

“Tangu ulipojitokeza siku ya kwanza nilikutabiria kuwa mgombea pekee na kweli nimekaa hapa kusubiri wee hakuna aliyetokea na hasa baada ya mtani wangu John Shibuda kuondoa nia yake ya kugombea kwa ridhaa yake kutokana na kuridhika na utendaji wako na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi…utabiri huo leo umethibitika,” alisema.

Alisema hakuna mwanachama aliyejitokeza hivyo ni uthibitisho kuwa wameridhika na utendaji kazi wake, imani waliokuwa nayo kwake na kwamba upo ushahidi wa kutosha ndiye mgombea pekee atakayepitishwa katika Uchaguzi Mkuu kwa kile alichomueleza kuwa ni mtaji wa CCM.

Katika hatua nyingine, Makamba alimfananisha Kikwete na Askofu ambaye ni mtumishi wa Mungu na kueleza kuwa kiongozi huyo ana sifa kama kiongozi huyo wa dini na kwamba anaamini anazo sifa za uanachama ambazo ni uongozi bora, hivyo kuna kila sababu ya kumchagua.

“Kwa miaka mitano umeonesha umahiri mkubwa, na nataka kukuambia kazi ya kukurudisha Ikulu ina wenyewe. Nawaambia wenzangu Rais wa Jamhuri ya Muungano ni Jakaya,” alisema na kuongeza kuwa uthibitisho mwingine ni wadhamini 14,069 aliowapata wakati alitakiwa kuwa nao 2,500 tu.

Wanachama wa CCM Makao Makuu katika risala yao iliyosomwa na Adamson Mwenesongole, walimpongeza Rais Kikwete kwa kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005-2010.

Walisema kitendo cha wanachama wengine kumuacha agombee ni kutokana na uaminifu na uadilifu wake na kuahidi kuungana naye kumpigia pipa badala ya debe ili apate ushindi wa kishindo.

Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania katika tamko lao, waliomba wanafunzi wote wamuunge mkono Kikwete kwa kupiga kura za ndio kwa maendeleo ya chama na taifa kwa ujumla.

Naye Mbunge wa Maswa, John Shibuda aliyeondoa nia yake ya kugombea urais, alisema alijiondoa baada ya kufanya upembuzi yakinifu na kuridhika na utendaji wa Rais Kikwete na kuongeza kuwa kamwe upepo hauwezi kuung’oa mchongoma na kwamba hiyo ndio salamu yake kwa wapinzani.

limchangia Rais Kikwete Sh 200,000 kwa ajili ya shughuli za uchaguzi ujao.

No comments:

Post a Comment

tubabarire ubanze wiyandikishe rwose!